ZABURI PART 01

| Makala

ZABURI:
Day 01


MLANGO 1
Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
2 Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
3 Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.
4 Sivyo walivyo wasio haki; Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
5 Kwa hiyo wasio haki hawatasimama hukumuni, Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki.
6 Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea.

 


MLANGO 2
Mbona mataifa wanafanya ghasia, Na makabila wanatafakari ubatili?
2 Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya Bwana, Na juu ya masihi wake.
3 Na tuvipasue vifungo vyao, Na kuzitupia mbali nasi kamba zao.
4 Yeye aketiye mbinguni anacheka, Bwana anawafanyia dhihaka.
5 Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake, Na kuwafadhaisha kwa ghadhabu yake.
6 Nami nimemweka mfalme wangu Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.
7 Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
8 Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
9 Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi.
10 Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili, Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe.
11 Mtumikieni Bwana kwa kicho, Shangilieni kwa kutetemeka.
12 Shikeni yaliyo bora asije akafanya hasira, Nanyi mkapotea njiani,Kwa kuwa hasira yake itawaka upesi,Heri wote wanaomkimbilia.


MLANGO 3
Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi, Ni wengi wanaonishambulia,
2 Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu, Hana wokovu huyu kwa Mungu.
3 Na Wewe, Bwana, U ngao yangu pande zote, Utukufu wangu na mwinua kichwa changu.
4 Kwa sauti yangu namwita Bwana Naye aniitikia toka mlima wake mtakatifu.
5 Nalijilaza nikalala usingizi, nikaamka, Kwa kuwa Bwana ananitegemeza.
6 Sitayaogopa makumi elfu ya watu, Waliojipanga juu yangu pande zote.
7 Bwana, uinuke, Mungu wangu, uniokoe, Maana umewapiga taya adui zangu wote; Umewavunja meno wasio haki.
8 Wokovu una Bwana; Baraka yako na iwe juu ya watu wako.

 

MLANGO 4
Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo; Umenifanyizia nafasi wakati wa shida; Unifadhili na kuisikia sala yangu.
2 Enyi wanadamu, hata lini utukufu wangu utafedheheka? Je! Mtapenda ubatili na kutafuta uongo?
3 Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa; Bwana atasikia nimwitapo.
4 Mwe na hofu wala msitende dhambi, Tafakarini vitandani mwenu na kutulia.
5 Toeni dhabihu za haki, Na kumtumaini Bwana.
6 Wengi husema, Nani atakayetuonyesha mema? Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
7 Umenitia furaha moyoni mwangu, Kupita yao wanapozidishiwa nafaka na divai.
8 Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara, Maana Wewe, Bwana, peke yako, Ndiwe unijaliaye kukaa salama.

 

MLANGO 5
Ee Bwana, uyasikilize maneno yangu, Ukuangalie kutafakari kwangu.
2 Uisikie sauti ya kilio changu, Ee Mfalme wangu na Mungu wangu, Kwa maana Wewe ndiwe nikuombaye.
3 Bwana, asubuhi utaisikia sauti yangu, Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia.
4 Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya; Mtu mwovu hatakaa kwako;
5 Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako; Unawachukia wote watendao ubatili.
6 Utawaharibu wasemao uongo; Bwana humzira mwuaji na mwenye hila
7 Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako, Nitaingia nyumbani mwako; Na kusujudu kwa kicho, Nikilielekea hekalu lako takatifu.
8 Bwana, uniongoze kwa haki yako, Kwa sababu yao wanaoniotea. Uisawazishe njia yako mbele ya uso wangu,
9 Maana vinywani mwao hamna uaminifu; Mtima wao ni shimo tupu, koo lao ni kaburi wazi, Ulimi wao hujipendekeza.
10 Wewe, Mungu, uwapatilize, Na waanguke kwa mashauri yao. Uwatoe nje kwa ajili ya wingi wa makosa yao, Kwa maana wamekuasi Wewe.
11 Nao wote wanaokukimbilia watafurahi; Watapiga daima kelele za furaha. Kwa kuwa Wewe unawahifadhi, Walipendao jina lako watakufurahia.
12 Kwa maana Wewe utambariki mwenye haki; Bwana, utamzungushia radhi kama ngao.


 SADAKA